Tuesday 14 March 2017

Rais Magufuli na Vitisho kwa Wabunge CCM

 

Rais John Magufuli ni sawa upande wake kuwatisha wabunge. Anafanya hivyo wabunge waogope kisha yeye na Serikali yake wawe na amani, watawale nchi bila kusumbuliwa.

Wabunge wao wanapaswa kujitambua na kukataa vitisho. Mbunge si mtetezi wa Serikali, bali mwakilishi wa wananchi. Mbunge ni polisi anayepaswa kuichunga Serikali.

Kama ambavyo polisi hutakiwa kuwa rafiki wa raia mwema, ndivyo ambavyo mbunge hupaswa kutokuwa na tatizo kwa Serikali inayotimiza wajibu wake vizuri.

Kama ambavyo polisi hupaswa kumbadilikia raia anapoona ametenda uhalifu, ndivyo mbunge hutakiwa kuwa mkali kwa Serikali anapoona inavuruga nchi.

Mbunge hapaswi kuwa mtetezi wa Serikali. Hakuna urafiki kati ya Bunge na Serikali. Hii ni mihimili miwili inayopaswa kusuguana kwa ajili ya maslahi ya nchi.

Mwananchi anatakiwa amwone mbunge wake ana kasoro pindi mbunge huyo anapogeuka 'shosti' wa Serikali. Mbunge kuwa rafiki wa Serikali maana yake amesaliti kazi iliyompeleka bungeni.

RAIS NA UENYEKITI WA CHAMA

Mambo ya wabunge CCM kutishwa ili waiogope Serikali, yatakoma pale CCM itakapoamua kutenganisha mamlaka mbili, Urais na Uenyekiti wa CCM.

Rais ndiye mkuu wa Serikali. Wabunge ndiyo wasimamizi wa Serikali.

Rais ndiye Mwenyekiti CCM, chama chenye wabunge wengi. Hivyo, anapoona wabunge wanatishia utulivu wa Serikali yake, anawafuata kwenye chama na kuwanyamazisha.

Kuhakikisha Bunge linakuwa chombo huru cha kutunga sheria, chenye kuisimamia, kuichunga na kuibana Serikali, vema mamlaka ya Serikali (Rais), itenganishwe na mamlaka ya chama (uenyekiti). Hii ni muhimu sana kwa nchi, usalama na ustawi wake. Siyo kwa CCM tu, bali kwa chama chochote kitakachokuja kushika dola. Rais wa nchi asiwe mwenyekiti wa chama chake.

Ndimi Luqman MALOTO

No comments:

Post a Comment